Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Hamid Maliki, Naibu Mkurugenzi wa Hawza ya Qum, aliyasema hayo katika kikao cha kuratibu maandalizi ya zoezi la ‘Kujitolea’ katika Mkoa wa Qum, kilichofanyika kwa kushirikisha maafisa wanaosimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali pamoja na viongozi wakuu wa mkoa huo.
Akizungumzia mwitikio mkubwa wa wananchi kwa kampeni ya Kujitolea, alisema: “Usajili mkubwa wa wananchi katika kampeni hii na kujitokeza kwao katika medani katika nyakati nyeti kumeonesha kwamba suala la Kujitolea si kauli mbiu au maneno ya kujigamba tu, bali linaonesha utayari halisi wa wananchi wa kuilinda nchi yao.”
Naibu Mkurugenzi wa Hawza ya Qum, huku akieleza kwamba kujitokeza wananchi katika medani wakati wanapohisi hatari ni ishara ya kuendelea kwa harakati ya wananchi yenye mwelekeo wa Mwenyezi Mungu, aliongeza: “Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi alikuwa amesema hapo awali kwamba ikiwa nchi itafanyiwa uchokozi, Mwenyezi Mungu atawaleta wananchi katika medani. Leo hii, tunashuhudia mifano ya kujitokeza na utayari huo ndani ya jamii.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Maliki, huku akizungumzia nafasi ya viongozi wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kuibua na kuendeleza harakati za wananchi na Muqawama, alibainisha: “Imamu Khomeini (ra), Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi na makamanda wakubwa kama Shahidi Haj Qasim Suleimani, kila mmoja alikuwa na nafasi muhimu katika kuanzisha na kupanua harakati hii. Juhudi na mapambano yao yaliweka msingi wa kuenea harakati za Muqawama katika ngazi ya kikanda na duniani kote.”
Akizungumzia msisitizo wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi kuhusu mabadiliko ya mfumo wa dunia na kupanuka Muqawama, alisema: “Mojawapo ya viashiria vya mabadiliko haya ni kupanuka Mstari wa Muqawama, ambao leo hii tunaona athari zake katika nyanja mbalimbali. “Wito wa kupinga ubeberu uliotolewa na Imamu Khomeini (ra), ambao wakati mmoja ulisikika kutoka katika Hawza ya Qum na Madrasa ya Feiziyah, bado unaendelea kusikika kama mwangwi duniani, na umesababisha kuibuka harakati zinazovuka mipaka ya Iran.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Maliki, akiishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuchukua msimamo wa kuunga mkono Mstari wa Muqawama, alisema kuwa; kushiriki katika kipindi hiki muhimu cha kihistoria ni fursa yenye thamani kubwa. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutambua majukumu yanayolingana na mazingira ya sasa.
Umuhimu wa kudumisha utayari na kuimarisha uwezo wa wananchi wa kuzuia uchokozi
Katika kuendelea na mazungumzo yake, alisema kuwa miongoni mwa mahitaji muhimu ya kufanikisha harakati za wananchi ni kudumisha utayari, kuboresha mbinu za kuwapanga na kuwaunganisha wananchi, pamoja na kuzingatia mahitaji yanayotokana na wakati na mahali. Alisema: “Ili kuhakikisha kwamba uwezo mkubwa wa wananchi unakuwa tayari wakati wote kujitokeza katika medani, ni lazima kuendelea kuimarisha utayari wao na kuhakikisha kwamba mazingira ya kuwawezesha wananchi kujitokeza kwa wakati yanabaki kuwepo pale inapohitajika.”
Naibu Mkurugenzi wa Hawza ya Qum, akizungumzia msisitizo wa Imamu Khomeini (ra) kuhusu kuundwa jeshi la watu milioni 20 na kupanuliwa nafasi za wananchi kushiriki, alisema: “Utayari wa jumla wa wananchi, ukiambatana na ufahamu, utambuzi sahihi wa mambo na mshikamano, unaweza kuwa na nafasi kubwa sana katika kuzuia uchokozi wa maadui. “Hii ni kwa sababu adui anapokabiliana na taifa lenye ufahamu na utayari, ambalo hujitokeza katika medani wakati wa hali nyeti, atakutana na vikwazo vikubwa katika kutishia au kulishambulia taifa hilo.”
Akizungumzia kuanza programu zinazohusiana na zoezi la ‘Kujitolea’ katika mikoa mbalimbali nchini Iran na kukaribia zamu ya kutekelezwa kwake katika Mkoa wa Qum, alisisitiza umuhimu wa kuandaa taasisi na vitengo vinavyohusika.
Aliongeza: “Vitengo vyote vinapaswa kujiandaa kutekeleza programu hii kulingana na majukumu na uwezo wake, huku vikihakikisha kwamba mazingira yanayohitajika kwa ajili ya wananchi kujitokeza kwa utaratibu na kwa wakati yanapatikana.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Maliki aliendelea kusema: “Ni muhimu kuifanya hali ya kuwa tayari kujitokeza katika medani kuwa utamaduni endelevu. Kwa namna hiyo, pindi kunapotangazwa haja ya wananchi kujitokeza na kubainishwa muda na mahali maalumu pa kukusanyika, taasisi na vitengo vinavyohusika vitaweza kushiriki kwa uratibu na utayari unaohitajika.
Naibu Mkurugenzi wa Hawza ya Qum, akihitimisha mazungumzo yake, alisisitiza kuwa: “Kama ambavyo mashahidi waliandika historia ya kishujaa kulingana na uwezo na nafasi zao, leo hii kila mtu anapaswa kuwa tayari, kwa kadiri ya uwezo wake, kuilinda nchi na tunu zake, na asisahau jitihada yoyote inayoweza kuchangia katika kutekeleza jukumu hili.”
Maoni yako